TAARIFA KWA UMMA KUHUSU UDAHILI WA WAOMBAJI WA MAFUNZO KATIKA PROGRAMU MBALIMBALI KWA NGAZI ZA ASTASHAHADA NA STASHAHADA KWA MUHULA WA MACHI/APRILI, 2018

BARAZA LA TAIFA LA ELIMU YA UFUNDI

(NACTE)

 

TAARIFA KWA UMMA KUHUSU UDAHILI WA WAOMBAJI WA MAFUNZO KATIKA PROGRAMU MBALIMBALI KWA NGAZI ZA ASTASHAHADA NA STASHAHADA KWA MUHULA WA MACHI/APRILI, 2018


Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) ni chombo kilichoundwa kwa Sheria ya Bunge, Sura ya 129, kwa lengo la kusimamia mafunzo yanayotolewa katika Vyuo vinavyotoa mafunzo kwa ngazi za Astashahada, Stashahada na Shahada ambavyo si Vyuo Vikuu ama Vyuo Vikuu Vishiriki nchini.

Jukumu mojawapo la Baraza, ni kuhakikisha kuwa mafunzo yanayotolewa katika Vyuo  vya Elimu ya Ufundi yanakidhi vigezo na ubora unaohitajika katika soko la ajira ndani na nje ya nchi.

Kwa muktadha huo, Baraza liliendesha zoezi la uhakiki wa Vyuo vinavyotoa elimu na mafunzo ya ufundi  kuanzia tarehe 27 Julai hadi tarehe 6 Septemba, 2017. Lengo kuu lilikuwa ni kuhakiki ubora wa mafunzo yanayotolewa pamoja na kubainisha changamoto zinazovikabili Vyuo hivyo katika utoaji wa mafunzo.

Katika uhakiki huo, Baraza lilibaini kuwa, baadhi ya Vyuo vilikidhi viwango vya ubora kwa mujibu wa taratibu za Baraza.  Hata hivyo, baadhi ya Vyuo vilibainika kuwa na changamoto mbalimbali zinazoweza kuathiri ubora wa elimu na mafunzo yanayotolewa.  Kufuatia zoezi hilo, Vyuo vyote vilivyobainika kuwa na mapungufu vilitaarifiwa na kutakiwa kurekebisha mapungufu yaliyobainishwa kabla ya kuendelea na udahili wa wanafunzi kwa mwaka mpya wa masomo 2018/2019.

Hivyo basi,  Baraza linautaarifu umma na waombaji wa nafasi za mafunzo kwa ngazi za Astashahada na Stashahada kwa muhula wa masomo wa Machi/Aprili, 2018 kuomba kwenye Vyuo vilivyokidhi ubora ambavyo vimeorodheshwa kwenye tangazo hili.

Aidha, Baraza linaelekeza kwamba Vyuo ambavyo havipo kwenye orodha iliyoambatanishwa hapa visidahili wanafunzi katika muhula wa masomo wa Machi/Aprili, 2018 bila kupata kibali cha Baraza kama ilivyoelekezwa.

Pia, Baraza linakumbusha kuwa udahili wa Muhula wa Machi/Aprili, 2018 hauhusishi programu zote za Kada ya Afya na Ualimu.

Kuona orodha ya vyuo vinavyokidhi vigezo bonyeza hapa

 

IMETOLEWA NA:

OFISI YA KATIBU MTENDAJI

BARAZA LA TAIFA LA ELIMU YA UFUNDI (NACTE)

TAREHE : 8 Machi, 2018

About Author

Leave A Reply

Send this to a friend