Fursa Za Ufadhili Wa Masomo Kwa Watanzania -Wizara Ya Mambo Ya Nje Na Ushirikiano Wa Afrika Mashariki

Taarifa Kwa Vyombo Vya Habari

Fursa Za Ufadhili Wa Masomo Kwa Watanzania

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imepokea fursa za ufadhili wa masomo ya muda mfupi na muda mrefu katika kada mbalimbali kutoka Serikali za Japan, China, Jamhuri ya Korea, Misri, Thailand, Denmark na Israel.

Kwa upande wa ufadhili wa masomo ya muda mfupi, Serikali ya Misri   imetoa nafasi kwa ajili ya Watanzania wote katika Sekta ya Teknolojia ya Uchakataji Madini (Minerals Processing Technology) itakayofanyika Cairo, Misri kuanzia tarehe 18 hadi 29 Machi, 2018. Mafunzo haya yanaratibiwa  na Wizara ya Madini.

Aidha, Serikali ya Tanzania imetoa mwaliko wa kushiriki mafunzo ya muda mfupi kwa Wastaafu yatakayofanyika Jijini Arusha kuanzia tarehe 19 hadi 30 Machi, 2018. Maombi ya ushiriki yaelekezwe Ofisi ya Rais, Menejimentii ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Vile vile Serikali ya Denmark imetoa mwaliko kwa Jeshi la Tanzania kushiriki kwenye mafunzo ya muda mfupi ya UNMILPOC yatakayofanyika kuanzia tarehe 09 hadi 27 Aprili, 2018. Mafunzo haya yanaratibiwa na Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

 

Kwa upande wa mafunzo ya muda mrefu, Wizara imepokea fursa za ufadhili wa mafunzo kwa ngazi ya Shahada ya Uzamili (Masters Degree) katika masuala ya Uchumi na Sera kutoka Chuo Kikuu cha Tsukuba kilichopo Japan. Mafunzo haya yanaratibiwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Pia, Serikali ya China imetoa fursa za ufadhili wa masomo kwa kipindi cha mwaka mmoja kwa ngazi ya Shahada ya Uzamili katika masuala ya Afya ya Jamii (International Master of Public Health-IMPH) kutoka Chuo Kikuu cha Tsinghua kilichopo Beijing. Mafunzo haya yanaratibiwa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

Wakati huohuo, Serikali ya China imetoa fursa ya ufadhili wa mafunzo kuhusu masuala ya Sheria za Kimataifa kutoka Chuo Kikuu cha masuala ya Nje cha Beijing. Mafunzo haya yanaratibiwa na Wizara ya Mambo ya Ndani na Wizara ya Katiba na Sheria.

Kadhalika,  Serikali ya China imetoa nafasi 80 za ufadhili wa mafunzo kwa ngazi ya Shahada ya Uzamili kwa Watanzania. Kati ya nafasi hizo 50 zinagharamiwa kwa kila kitu na nafasi 30 hazitagharimiwa kwa kila kitu. Vile vile Serikali hiyo itatoa nafasi 20 kwa ajili ya kozi za Nishati na Madini. Mafunzo haya yanaratibiwa na Wizara ya Elimu, Sayansi, na Teknolojia, Wizara ya Madini na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Katika hatua nyingine, Serikali ya Jamhuri ya Korea imetoa nafasi tatu (3) za fursa za ufadhili wa mafunzo kwa ngazi ya Shahada ya Uzamili katika Taasisi ya Taifa ya Elimu ya Kimataifa iliyopo nchini Korea. Maombi yatumwe kupitia anuani ifuatayo: www.gradadmission.tshinghua.cn/f/login.  Mafunzo haya yanaratibiwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Kwa upande wa Serikali ya Thailand imetoa ufadhili wa mafunzo ya miaka miwili kwa ngazi ya Shahada ya Uzamili na Diploma kwa Watanzania.

Pia, Serikali hiyo imetoa mwaliko wa kushiriki mashindano ya kuandaa andiko kuhusu “Share it with TICA on the Topic Related to Sufficiency philosophy for Sustainable Development”. Andiko hilo liwe tayari tarehe 31 Machi, 2018 na liwasilishwe kupitia anuani ifuatayo: TICAArticleContest@gmail.com.  Mafunzo yanaratibiwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma.

Kutoka Serikali ya Israel, Wizara imepokea mwaliko kwa Watanzania kushiriki mafunzo kwa ngazi ya Shahada ya Uzamili kuhusu Maendeleo ya Mtoto. Mafunzo yanaratibiwa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto.

 

Imetolewa na:

Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,

Dar es Salaam

08 Machi, 2018

About Author

Leave A Reply

Send this to a friend